Kila mchoraji kabla ya kuchora picha huwa na taswira
ya picha hiyo akilini mwake, kisha huamua kubadili taswira ile kuwa mchoro.
Ndivyo yalivyo maisha yetu ya kila siku, akilini mwako unakuwa na ndoto nyingi
za maisha ambazo kwa muda huo ni taswira tu iliyopo akilini mwako unahitaji
kuamua na kuchukua vifaa na zana na kuanza kubadili taswira hiyo kuwa mchoro
halisi yaani upange mipango na kuitekeleza ili ufikie ndoto zako za kimaisha.
Kila mtu akilini mwake ana taswira ya pekee ya
maisha anayoyapanga na kuyapigania ili ayafikie. Kama ilivyo kwamba mchoraji
hawezi kuwa na taswira au kuchora kituambacho hajawahi kusikia wala kuona vivyo
hivyo katika maisha ya binadamu taswira ya maisha yako hujengwa na taarifa
unazozijua au kuzisikia kuhusu maisha.
Ubora wa taswira uliyonayo kichwani hutegemea taarifa ulizonazo juu ya
maisha kama una taarifa sahihi kuhusu maisha basi akili yako pia itajenga
taswira bora ya maisha na vivyo hivyo hujenga taswira isiyo na ubora kama huna
taarifa za kutosha juu ya maisha. Je, una taarifa sahihi zitakazokuwezesha
kujenga taswira bora ya maisha yako?
Kumbuka;
huwezi kupata taarifa sahihi pasipo kujifunza kutoka kwa watu waliokutangulia
na kusoma vitabu ili kupata maarifa na ujuzi wa kutosha kuweza kujenga taswira
bora na hatimae kuwa na maisha bora.
Kama ilivyo katika uchoraji viwango vya uchoraji
hutofautiana, vivyo hivyo katika maisha yetu mafanikio hutofautiana. Kuchora
chini ya viwango haimaanishi hukuwa na taswira bora tu bali pia unaweza
ukashindwa kuiwasilisha taswira nzuri uliyokuwa nayo akilini mwako na kuibadili
kuwa mchoro halisi. Huenda ni kuchanganya rangi au vifaa vinavyohiitajika
wakati wa kuchora lakini hiyo tu ikafanya picha ionekane haina ubora. Katika
maisha unaweza kuwa na taarifa sahihi na kujijengea taswira nzuri na bora ya
maisha lakini ukashindwa kuibadili na kuifanya kuwa maisha halisi. Huenda ni
kutokana na kukata tama, uvivu, kughairi na hata kushawishiwa na watu wengine
kubadili mwelekeo wako. Ndugu kuwa na taswira bora tu sio kufikia mafanikio, ni
wengi sana wana mawazo mazuri ya biashara, mipango mizuri ya maisha lakini
wanashindwa kuibadili kuwa maisha halisi na kuishia kuyeyuka kwa taswira hizo
akilini mwao.
Hatua hii ya kuweza kubadilisha taswira iliyojengeka
akilini na kuwa maisha halisi ndio huweka tofauti kati ya watu wanaofanikiwa na
wasiofanikiwa. Kubadili taswira kuwa maisha halisi ni hatua inayohitaji nguvu,
akili na moyo wako wote ili kuweza kupata picha halisi ya taswira yako.
Haya ni mambo muhimu manne yatakayokusidia kubadili
taswira uliyoijenga kichwani mwako kuwa maisha halisi.
1. Kuambatana na watu sahihi. Watu sahihi ni wale
watu ambao mnamipango inayoendana na mawazo yanyorandana, watu ambao
watakunyanyua na kukutia moyo pale unapoanguka au kukata tama.
2. Kugawa mipango yako katika sehemu ndogo ndogo;
mchoraji huanza kuchora sehemu zile zinazomsumbua na taratibu huunganisha na
kupata picha halisi ya fikra zake. Vivyo hivyo katika maisha usiende pupa, anza
na sehemu ndogo ndogo ambazo ni ngumu kwako, kisha ukija kuuganisha utapata kitu
halisi. Pia kuugawa mpango katika sehemu ndogo ndogo husaidia mtu usighairi
kwakuwa kazi inakuwa ndogo na unaweza kufanya kipande kidogo ukakamilisha.
3. Kujipa
morali ya kusonga mbele; kukata tamaa ni moja ya mambo yanayofanya watu
washindwe katika maisha. Ili kuepuka kukata tama unatakiwa kujikumbusha na kuangalia
mwenendo wa malengo yako mara kwa mara na pia kujipongeza pale unapofanya
vizuri, usingoje kupongezwa na watu wengine kwani hakuna anaejua taswira
iliyopo akilini mwako.
4. Endelea
kujifunza na kuongeza maarifa kila siku; elimu haina mwisho maarifa mapya
huvumbuliwa kila iitwapo leo. Hivyo hatuna budi kujifunza maarifa na ujuzi mpya
kila siku ili tuweze kuendana na mabadiliko yanayotokea kila siku.
ANZA LEO KUBADILI TASWIRA YA MAISHA ULIYOIJENGA AKILINI MWAKO KUWA MAISHA HALISI.

Comments
Post a Comment