Kila jambo unalolifanya duniani linakuwa na asilimia kadhaa
ya kushindwa, ndio maana watu huwa na plani B. Unaweza kufanya jambo kwa
uhakika kabisa lakini kitu kidogo sana kikakufanya ushindwe, na hii ndio
inafanya watu wafanye vitu kwa umakini na kufikiria sana hasa pale ambapo
unania ya kufanikiwa katika mambo yako. Lakini muda mwingine unaweza kuwa
umefanya jambo kwa umakini sana bila kukosea lakini ukashindwa kwasababu za mtu
mwingine ambae mlikuwa mnashirikiana nae huenda ni kwa uzembe au bahati mbaya
lakini mambo ndio yameharibika.
![]() |
| Lawama |
Katika hali kama hii ndipo watu huanza kutupiana lawama,
huyu anamwambia mwingine “Unaona uzembe wako umetutia hasara”, Yule pia
anatafuta sababu ya yeye kukosea, anaweza akatupia mpira kwa mwingine au la
akalaumu vifaa alivyotumia au miundombinu, ilimradi asionekane mkosaji. Katika
kampuni au madaraka Fulani watu hupenda kuwatupia lawama watu wa chini yao
kimadaraka, lawama hizi huenda ngazi kwa ngazi mpaka kumfikia mtu wa mwisho kimadaraka
ambae nae hujaribu kutafuta mbinu ya kuonekana sio mkosaji hivyo kuamua kulaumu
mazingira ya kutendea kazi au vifaa ambavyo haviwezi kujitetea.
![]() |
| Kila mmoja humtupia lawama mwenzie |
Tabia hii humfanya mtu kuyakwepa majukumu yake na kupelekea
kupunguza upeo wake wa kufikiri katika kutatua matatizo, yeye kila tatizo
linapokuja akishindwa hutafuta kisingizio. Hii tabia ikijijenga ndani yake
hufanya mtu kujiona hana hatia hata pale anapokosea na kupelekea uzembe ambao
huzaa uvivu na hatimae umasikini.
Je, suluhisho ni lipi?
ACHANA NA LAWAMA ANZA KUWAJIBIKA KWA KILA KOSA HATA KAMA
HUJALISABABISHA WEWE MOJA KWA MOJA.
![]() |
| Jilaumu mwenyewe |
Kosa lolote linapotokea katika mazingira yako au jamii yako
lazima wewe unahusika iwe kwa moja kwa moja au kwa namna moja ama nyingine
unahusika, hivyo CHUKUA WAJIBU KWA KILA TATIZO.
Mfano umeshindwa kukamilisha mpamgo Fulani kiuchumi
kwasababu mtu uliemkopesha pesa yako amechelewa au anazungusha kukulipa pesa
yako, basi usilaumu kwani wewe pia unawajibika. Kosa lako ni kumwamini mtu ambae si mwaminifu, pia kukopesha pesa
ambayo ipo kwenye mipango muhimu, hivyo unatakiwa ukae chini uelewe kosa lako,
pata somo katika lile kosa, wakati mwingine hutarudia tena kosa hilo.
Huenda umenunua kifaa cha ofisini kikawa hakifanyi kazi kama inavyohitajika basi jua ulikosa umakini wakati unanunua hivyo
wakati mwingine fanya utafiti kabla ya kufanya manunuzi ya vifaa vyako.
Huenda una rafiki ambae amekusababishia matatizo makubwa
katika maisha yako, kaa chini fikiria ulikosea wapi, jifunze, tafakari siku
nyingine ufanye nini kuepuka kosa kama hilo.
Mwandishi Brian Tracy katika kitabu chake cha Just Shut up
and Do It, anasema lawama huleta mawazo mabaya akilini mwa mtu na humfanya aone
kuna watu wengine wanaowajibika na maisha yake, jambo ambalo sio sahihi. Hivyo
ili kuondokana na mawazo mabaya pamoja na utegemezi kila unapokutana na
changamoto jitamkie “NI WAJIBU WANGU”, hii kauli huamsha akili na kufikiria juu
ya suluhisho la hilo jambo.
Maisha ni yako wewe WAJIBIKA KWA kila suala
linalokukabili/linalokutatiza, hakikisha kila changamoto inayokukabili
unafikiria wewe binafsi unaweza kufanya nini kutumia kile ulichonacho kama mtu
mwingine pia atatatua kwa upande wake ni jambo la heri. Kujijengea tabia ya
kutatua kila chamgamoto inayokukabili na kuwajibika kwa kila kosa linalotokea, hujenga
uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo kwa haraka na hivyo kukufanya ufanikiwe
katika mipango yako mingi.
NAKUTAKIA UTEKELEZAJI MWEMA.
Usichoke Kujifunza.



Comments
Post a Comment