Maisha ya mtafutaji ni
ya mateso, shida na raha ambavyo vyote kwa pamoja vina mchango mkubwa wa
kukusogeza mbele ili ufikie malengo yako. Hakuna maisha yenye mateso na shida
tupu na wala hakuna maisha ya raha pekee, hii ni kwa matajiri, fukara na hata
wale wa uchumi wa kati. Tofauti yetu ni aina ya shida na matatizo tunayokutana
nayo, maskini ana shida zake anazopambana nazo ambazo tajiri anaona si kitu
kwake, vivyo hivyo tajiri nae ana shida
zake ambazo maskini huona si kitu.
Katika kupita kwenye
hizi shida, raha na matatizo mbalimbali mtu usipokuwa makini unaweza ukapoteza
uelekeo wako au kuahirisha safari yako kuelekea kwenye mafanikio. Napoleon Hill
mwandishi wa kitabu maarufu cha Think and
Grow Rich aliwahi kuulizwa kwanini watu wanashindwa kufanikiwa, Hill
alijibu akasema kuna mambo matatu yanayofanya mtu asifanikiwe 1; Kushindwa
kuendana na watu (jamii inayomzunguka) 2; Kuahirisha na 3; Kuacha kufanya jambo
(kughaili). Lakini mimi naomba nikuongezee jambo jingine nalo ni
KUDANGANYIKA NA VITU VIZURI NJIANI katika safari yako kuelekea mafanikio.
Sio kila mahali ambapo
unapopafurahia ndio mahali sahihi kwako nyingine ni danganya toto. Kama maishani
mwako umelenga kufikia mahali Fulani njiani utapita sehemu nyingi ambazo
zitakufurahisha na kukupendezesha na kama hauko makini unaweza kudhani ndio
umefika mwisho wa safari yako, la hasha umedanganyika tu. Unaweza kuajiriwa
katika kampuni ambayo ikakupa mshahara na mkataba mnono sana hadi ukapumbazika
kwamba wewe pale unapita na safari yako ni ndefu, pia yawezekana rafiki yako
kakueleza mpango mzuri wa kuingiza pesa nyingi kwa kazi rahisi na kwa muda
mfupi ukadanganyika na kusahau safari na malengo yako. Inawezekana pia mzazi
wako akakurithisha mali nyingi kiasi cha kukupumbaza wewe kusahau malengo yako.
Siku zote mahali ambapo
si pako hapatakufaa siku zote, kama ule msemo wa Kiswahili usemao Nguo ya kuazima haisitiri mwili, ipo
siku utatambua kuwa sio mahali pako sahihi au yale mazuri ya sehemu hiyo
yakaisha au kupungua. Kama ni kampuni huenda likafilisika au ukafukuzwa kazi na
kama ni mali za urithi ukashhindwa kuendeleza kwani sio mahali sahihi
unapotakiwa wewe kuwepo. Lazima kama mtu uliejizatiti kutimiza malengo yako
uweze kutambua na kutofautisha kufikia malengo yako na kudanganyika na tama za
njiani.
Tamaa za njiani ni
chanzo kikubwa cha kukufelisha katika mipango yako, tamaa hizi lazima
zitakuchelewesha kufikia malengo yako au kukupoteza kabisa na kukufanya
ushindwe kufikia malengo yako. Mtu aliejizatiti katika kutimiza malengo yake lazima
atakuwa makini sana atakutana na sehemu nzuri za kutamanisha lakini atajua ni
za kupita na hawezi kupoteza mda akijihusisha nazo. Tambua mwisho wa safari
yako, itakusaidia kuepuka tamaa za njiani.
MUNGU AKUONGOZE NAMNA YA KUTAMBUA SEHEMU YAKO SAHIHI.
MUNGU AKUONGOZE NAMNA YA KUTAMBUA SEHEMU YAKO SAHIHI.

Comments
Post a Comment