Umewahi kujiuliza ni kitu gani cha pekee ambacho
kinakutambulisha katika jamii unayoishi?. Kuna watu katika jamii yoyote
wanakuwa maarufu kwa tabia au matendo ya tofauti, wakati mwingine wanapewa
mjina ya utani kutokana na matendo au tabia hizo. Ukiwachunguza kwa makini hata
katika utendaji wao wa majukumu mbalimbali huwa ni wa tofauti sana na watu
wengine, wao mara nyingi huwa na upekee katika mambo yao. Je, wewe utofauti
wako ni upi katika matendo, mawazo, na malengo yako?
Katika nyakati hizi ambazo utandawazi na tekinolojia
vimetawala sana, habari na taarifa zinaenea kwa haraka sana na kufanya mambo
mengi kuwa ya wazi zaidi, ushabiki wa watu maarufu umeongezeka na kuenea sana.
Katika mambo ambayo yameenda sambamba na kuenea na kukua kwa utandawazi ni KUIGA/KUFUATISHA.
Watu wengi wamekuwa wakifanya mambo kwa kuiga au kufuata watu maarufu au watu
wengine wanaowaamini, muda mwingine mpaka watu wanashindwa kuwatofautisha
kuanzia mavazi mpaka matendo mtu anaiga.
Kuna usemi niliuandika katika somo la MAMBO MUHIMU KWAKO KIJANA WA LEO unaosema Albert
Einstein aliwahi kusema “The woman who follows the crowd will usually go no
further than the crowd. The woman who walks alone is likely to find herself in
place no one has ever been before” (mwanamke anaefuata kundi hawezi kwenda
mbali zaidi ya lile kundi. Mwanamke anaetembea pekeake anaweza kufika mahali
ambapo hakuna mtu aliewahi kufika pale kabla). Angali watu waliofanikiwa wengi
walifanya mambo ya tofauti nay a kipekee; Mfano tajiri wa kwanza duniani kwa
sasa aliamua kuacha chuo cha Harvard (moja kati ya vyuo bora duniani) mwaka
1975 akiwa na miaka 20 na kuanza kujihusisha na mambo yake mwenyewe. Hivyo ili
ufanikiwe lazima ufanye kitu ambacho ni tofauti na wengine na utafika mahali
ambapo wengine hawajafika na hayo ndio mafanikio.
Katika jamii yoyote kuna mtu anaefahamika sana kutokana na
umbo lake (Mnene, Mfupi, mweupe kuliko wote n.k) au kutokana na matendo yake,
tabia yake ya kipekee na kadhalika. Ukiwa kipekee lazima watu watakufahamu
popote uendapo, kile kitu cha kipekee kitakuwa ni alama ya utambulisho wako kwa
wengine. Kufahamika ni moja ya nyenzo au silaha muhimu kwa mtu unaeanza
kupigana kuelekea mafanikio yako. Kumbuka lazima uwe mtu wa pekee ili uweze
kufahamika na kujenga heshima katika jamii yako.
Mtu yeyote katika dunia anakuwa na malengo na ndoto ambazo
anapenda zitimie, ndoto ulizonazo wewe hazifanani na ndoto za mtu mwingine hata
kama mtafanana malengo yenu. Kila mmoja anafikiria na anafanya juhudi ili
kuifikia ndoto yake ya maisha. Ndugu, ukiishi kwa kuiga anachofanya mtu fulani
huwezi kufikia ndoto yako ya maisha, utaishia kupotea kwakuwa huyo unaemfuata
matendo, tabia au ratiba yake hujui ndoto yake wala fikra zake. Unahitaji
kuishi maisha yako halisi, ufuate ndoto yako na hapo utaona namna unavofanikiwa
na kufikia ndoto zako. Ili utimize ndoto na malengo yako lazima uiishi nafsi
yako kuanzia matendo, tabia, na ratiba yako. Lazima uthamini mawazo na fikra
zako mwenyewe, lazima uwe na mtindo wako.
Vijana wengi kwa sasa wamerundikana katika fani za usanii na
utumbuizaji, hata vijana wengine wenye elimu ya juu waliokosa ajira
wamekimbilia huko. Baadhi ya vijana wamebaki mitaani wakisubiri kazi huku
wakijiuliza VIPAJI VYAO NI VIPI??. Haya yote yanatokana na kuishi maisha ya
kuiga au kufuata mtu Fulani, huenda kwa sasa humfuati wala kuiga mtu yeyote
lakini kuna mtu ulikuwa unamfuata na sasa unatambua umeshapoteza njia kuelekea
kwenye ndoto na malengo yako. Huwezi kutambua kipaji chako kama unaishi kwa
kumfuata maisha ya mtu mwingine, lazima utapotea na ukija kutambua umeshachelewa
na umri umeenda. Ishi maisha yako ishi
nafsi yako ili uweze kutambua na kumudu kipaji chako.
Ben alikuwa ni mwanafunzi katika shule moja ya sekondari ambae alikuwa na
malengo na ndoto zake za kutimiza katika maisha yake. Shule hiyo ilikuwa ni ya
bweni akawa akiamka asubuhi saa kumi alfajiri anaenda darasani na kusoma hadi
saa kumi na mbili anarudi bwenini na kujiandaa kwaajili ya kuingia darasani
kama wanafunzi wengine. Hiyo ikawa ndio ratiba yake ya kila siku, lakini kila
siku akiingia darasani saa kumi alfajiri alikuwa anamwona kijana mmoja
anajisomea, akajua huyo mwanafunzi anajisomea masomo ya shule hivyo
hakumfuatilia kwakuwa yeye alikuwa akijisomea vitabu vya masomo ya maisha
hasahasa vitabu vya ujasiriamali, ufugaji na kilimo cha kisasa.
Siku moja Ben
aliamka alfajiri na mapema na kwenda darasani kama kawaida yake alipofika
hakumwona Yule mwanafunzi aliezoea kumwona anawahi kila siku, lakini Ben
hakujali alifungua kitabu chake na kuanza kusoma. Nusu saa baadae Yule
mwanafunzi aliingia na kumkuta Ben alishawahi kufika, alipita alipo Ben na
kumpa salamu na kwenda kukaa kwenye kona ya darasa kama mazoea yake ya kila
siku. Ben aligeuka kumwangalia vizuri Yule mwanafunzi sio kwamba alikuwa
hamfahamu, la hasha kuna kitabu alimwona amekibeba na kilikuwa ni moja ya
vitabu anavyovitafuta sana. Aliamua kusimama na kumfuata Yule mwanafunzi na
kuanza kuzungumza nae. Kila mmoja akatambua malengo ya mwenzake kuwa nje ya
masomo muda wa alfajiri wote huwa wanajisomea masomo ya ziada, ukawa ni mwanzo
wa wao kuwa na ukaribu kuazimana vitabu na majadiliano ya maada mbali mbali.
Kwa sasa Ben anamiliki kampuni ya kusindika mzao mbalimbali na rafiki yake ni anamiliki
kampuni ya usafirishaji aliyorithi kwa baba’ke.
Umejifunza nini katika hadithi hii fupi?
Ukiishi maisha yako halisi na kufanya juhudi za kufikia
malengo yako, katika harakati zako utakutana na watu wanaoendana na malengo
yako, utakutana na marafiki ambao wanafanana ratiba na malengo, hiyo
itakusaidia kukupa moyo na kukutia hamasa ya kuzidi kusonga mbele.
MAWAZO, MALENGO NA JUHUDI PEKEE HAVITOSHI KUTIMIZA NDOTO ZAKO,
TANGULIZA SALA KWA MUUMBA WAKO.
TANGULIZA SALA KWA MUUMBA WAKO.



Comments
Post a Comment